Abstract:
Tanzu za riwaya na hadithi fupi kimsingi huandikwa ili kusomwa, bali siyo kuigizwa. Kwa muda wa miaka kumi na mitano hivi wasimilishaji wamefanya juhudi kuigiza tungo za kinathari za fasihi ya Kiswahili. Hali ya kuziigiza tungo za kinathari hutokana na ugeuzaji wa vipengele fulani vya kinathari ili vichukue umbo la kitamthilia. Lengo la uchunguzi huu lilikuwa kutathmini usimilisho wa riwaya na hadithi fupi kwa wanafunzi wa sekondari nchini Kenya. Uchunguzi ulidhamiria kubainisha dhana, historia, mbinu na matatizo ya usimilisho, na kupendekeza njia za kuyatatua matatizo hayo. Uchanganuzi umebainisha kwamba riwaya na hadithi fupi husheheni sifa za kitamthilia ambazo huwa msingi wa usimilisho. Aidha, imebainika kwamba mchakato wa kuubadilisha muundo wa kinathari na kuufanya wa kitamthilia huandamana na changamoto ambazo kama hazishughulikiwi ipasavyo zinaweza kuzalisha matatizo ya usimilisho. Uchanganuzi wa data uliongozwa na nadharia changamano iliyohulutisha misingi ya nadharia ya usimilisho na ya uigizaji. Mkabala wa nadharia ya usimilisho ulioongoza uchunguzi huu huhimiza usimilisho ufanywe kama tafsiri, pale maana ya matini chasili huhamishwa kwa usahihi iwezekanavyo. Hii ni kwa sababu usimilisho wa tungo zinazotahiniwa katika mtihani wa KCSE hutarajiwa kuwa na usahihi wa matini chasili. Misingi ya nadharia ya uigizaji ilitumika kutathmini ufaafu wa mbinu zilizotumika kusimilisha matini ya riwaya na hadithi fupi kwa muundo wa kitamthilia. Tasnifu hii imetumia mbinu changamano za utafiti ambapo mikakati ya kijarabati na kimaelezo imetumika kukusanya, kuchanganua, na kuwasilisha data. Utafiti ulifanywa katika magatuzi ya Nairobi na Kitui ukihusisha vikundi vinne vya uigizaji. Vikundi hivyo vilisimilisha riwaya za Utengano na Siku Njema, na diwani za hadithi fupi za Mayai Waziri wa Maradhi na Hadithi Nyingine na Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine. Uchunguzi umebaini kwamba mbinu zilizotumika kusimilisha riwaya na hadithi fupi kuwa matini za kitamthilia zilikuwa za kimwingiliano matini. Kutegemea stadi za wasimilishaji katika matumizi ya mwingiliano matini, usimilisho ulijitokeza kama aminifu ama uliokengeuka kwa matini chasili. Riwaya na hadithi fupi zilizohakikiwa masimilisho yake zilidhihirisha uwepo wa sifa za kitamthilia ambazo ndizo kiini cha ubunaji wa mbinu za usimilisho. Fauka ya haya, tungo za kidrama na kinathari hubuniwa kwa sifa fulani za kimfanano ambazo huifanya rahisi kwa msimilishaji kuugeuza utanzu mmoja kuwa mwingine. Hizi ni sifa za mwingiliano matini. Katika mjadala wa mwingiliano matini, utafiti huu umebainisha kwamba, matini zinaweza kuingiliana na zikadumisha sifa zake asilia, kinyume na inavyodaiwa na wahakiki wa mwingiliano matini.